Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi 36 duniani ikiwemo DRC hazina kabisa mashine ya tiba dhidi ya saratani

Nchi 36 duniani ikiwemo DRC hazina kabisa mashine ya tiba dhidi ya saratani

Mataifa 36 duniani hayana mashine za kutoa huduma ya kutibu saratani, limesema shirika la kimataifa la nishati ya atomiki, IAEA katika taarifa yake inayoweka bayana uwepo wa mashine hizo maeneo mbali mbali duniani.Brian Lehander na taarifa zaidi.

(Taarifa ya Brian)

IAEA imechapisha orodha ya upatikanaji wa mashine hizo katika vituo vya kutoa tiba za saratani ulimwenguni ambapo Marekani inaongoza kwa kuwa na mashine zaidi ya Elfu Tatu Mia Mbili, huku baadhi ya nchi kama Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC ikionekana kuwa na mashine moja lakini nayo haifanyi kazi.

Mkuu wa kitengo cha takwimu hizo cha IAEAJoanna Izewska amesema taarifa hizo ni kutoka nchi 141 na zinaonyesha maeneo ambako wagonjwa wa saratani hawawezi kupata huduma kabisa na hivyo ni fursa ya kuwezesha kupanga vyema huduma za tiba dhidi ya saratani katika nchi zinazoendelea.

Amesema ni dhahiri kuwa licha ya juhudi za miongo kadhaa za kuimarisha huduma dhidi ya saratani, bado hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha huduma ya tiba inapatikana kwa watu wengi zaidi.