Surua haiko tena ukanda wa Amerika- WHO/PAHO
Ukanda wa Amerika umekuwa wa kwanza duniani kutokomeza surua, ugonjwa unaoweza kusababisha matatizo makubwa ya afya kama vile vichomi, upofu, ubongo kuvimba na hata kifo.
Mafanikio haya yamepatikana baaada ya miaka 22 ya kampeni za chanjo dhidi ya surua, rubella na matumbwitumbwi kwenye ukanda huo.
Tamko la kutokomezwa surua limetangazwa wakati wa kikao cha 55 cha baraza la uongozi la shirika la afya duniani WHO na lile la afya ukanda wa Amerika, PAHO.
Akizungumza baada ya tangazo hilo, mkurugenzi wa PAHO Carissa F. Etienne amesema ni siku ya kihistoria kwa ukanda wa Amerika na dunia nzima kwa ujumla, akisema kuwa ni ushahidi wa mafanikio ya aina yake ambaye yanaweza kupatikana nchi zikifanya kazi pamoja na kwa mshikamano katika lengo moja.
Kabla ya kuanza kwa kampeni za chanjo mwaka 1980, surua ilikuwa ikisababishwa karibu vifo milioni 2.6 kila mwaka duniani kote, ambapo ukanda wa America ulikuwa vifo zaidi ya Laki moja kati ya hivyo kati ya mwaka 1971 na 1979.