Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjadala wa wazi wa Baraza Kuu wafunga pazia

Mjadala wa wazi wa Baraza Kuu wafunga pazia

Baada ya siku sita za mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, hatimaye pazia limefungwa ambapo viongozi wa nchi, serikali na wawakilishi walitoa hotuba zao kuwekea msisitizo masuala ya msingi katika kuendeleza amani, usalama, maendeleo na haki za binadamu.

Rais wa Baraza hilo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na mwakilishi wa Nepal katika Umoja wa Mataifa Balozi Durga Bhattara ameangazia masuala ambayo yalipatiwa kipaumbele na nchi wanachama ikiwemo wakimbizi, marekebisho ya muundo wa baraza la usalama bila kusahau tabianchi.

Wakati wa mjadala huo nchi zaidi ya 31 ziliridhia mkataba wa Paris na hivyo amesema..

“Nimeona kuwa sasa tunahitaji uridhiaji wa mkataba utakaowezesha kuziba pengo la asilimia 7.5 za hewa chafuzi zinazotolewa ili mkataba uweze kuanza kutumika. Natumai tutashuhudia hilo kabla ya mkutano wa COP22 huko Morocco."

Na kama hiyo haitoshi akasema..

“Nasihi nchi zote wanachama siyo tu waridhie mkataba haraka, bali pia waongeze matamanio yao ya kupunguza utoaaji wa hewa chafuzi ili kiwango cha ongezeko la joto duniani kisizidi nyuzi joto 1.5 katiak selsiyasi, na pia kuhamasisha uchangiaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya kusaidia nchi ambazo ziko hatarini zaidi mfano nchi za visiwa vidogo na nyinginezo.”

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson alimwakilisha Katibu Mkuu Ban Ki-moon, naye akapazia sauti suala la wakimbizi na umuhimu wa mikutano ya ngazi ya juu kuhusu wakimbizi na wahamiaji akisema zaidi ya yote..

(Sauti ya Eliasson)

Tunapaswa kuhakikisha kuwa shirika hili linatuma ujumbe kwamba kila mtu ana thamani sawa na tunahitaji kufanya kazi ili kuzuia mienendo ya chuki dhidi ya wageni haiendelei, mienendo ambayo kwa sasa imeimarika sana.”