Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkataba wa amani Colombia kutiwa saini kwa “kalamu ya risasi”

Mkataba wa amani Colombia kutiwa saini kwa “kalamu ya risasi”

Muafaka wa kihistoria wa amani baina ya serikali na majeshi ya mapinduzi ya Colombia FARC, utatiwa saini kwa ‘kalamu ya risasi” umesema mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo .

Kwa mujibu wa duru za habari, kalamu hizo zimetengenezwa kwa idhini ya serikali kama ishara ya amani na kukumbusha haja ya kuwekeza katika elimu.

Mkataba huo unamaliza miaka 50 ya vita Colombia. Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon, yuko kwenye mji wa mwambao wa Cartagena ili kuhudhuria hafla ya utiaji saini mkataba huo unaomaliza miongo mitano ya machafuko.

Ban pia atapewa kalamu ya risasi kama kumbukumbu ya tukio hilo. Baada ya utiaji saini huo Ban atakutana na kamanda wa kundi la FARC Timoleon Jimenez ambaye anajulikana pia kama "Timochenko".

Muafaka baina ya FARC na uongozi wa Colombia utahitaji kuidhinishwa na kura ya amani ya kitaifa itakayofanyika mwezi Oktoba.