Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi Sudan Kusini wahamishwa kwa ajili ya usalama wao

Wakimbizi Sudan Kusini wahamishwa kwa ajili ya usalama wao

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi(UNHCR) limesema, limeanza operesheni ya kuhamisha wakimbizi wa ndani wa Sudan Kusini walio hatarini zaidi kutoka kwenye mji wa Yei na kuwapeleka kwenye kambi ya kitongoji cha Lasu nchini humo.

Wakimbizi waliohamishwa kuanzia Jumatano kutoka Yei ni 644 kati ya 1,499, wengi wao wakiwa ni wakina mama ambao wanashindwa kumudu maisha yao na ya familia zao kutokana na umasikini uliokithiri na hali mbaya ya kiuchumi. UNHCR imesema imelazimika kuwahamisha wakimbizi hawa haraka kwani wamo hatarini kutumia njia zingine zisizo halali kulipa kodi au kuwalipia watoto shule.

Pindi wanapowasili Lasu, wakimbizi hawa wanapata chakula, vifaa vya kilimo na ardhi kwa ajili ya kujenga nyumba, na wakina mama wanaonyonyesha wanapata malazi, chakula, huduma za afya na elimu.

Kambi ya Lasu ilianzishwa mwaka 2009 kuwahifadhi wakimbizi kutoka Congo waliokimbia waasi wa LRA na hadi sasa inahifadhi wakimbizi 265,235.