Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ahadi za utekelezaji wa mkataba wa amani Mali zimeishia kuwa hewa:Ban

Ahadi za utekelezaji wa mkataba wa amani Mali zimeishia kuwa hewa:Ban

Mkutano wa Mawaziri kuhusu utekelezaji wa mkataba wa amani nchini Mali, umefanyika leo hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa, ambapo umehudhuriwa na Rais wa Mali, Ibrahim Keita na wadau wengine, pamoja na Katibu Mkuu Ban Ki-moon.

Amesema, ingawa hatua zote za kuimarisha utawala wa sheria kama taasisi za usalama na huduma zingine za msingi zimetolewa nchini Mali, lakini utekelezaji wa mkataba huo ulioafikiwa mwaka uliopita, bado umekuwa finyu mno, na kusema

(Sauti ya Ban)

"Tunaona uhasama na ukiukwaji wa mkataba wa kusitisha mapigano. Ni mwezi uliopita tu, nimelaani vikali mapigano baina ya vyama vilivyosaini mktaba huo Kidal. Na tena, kulikuwa na mapigano mapya wiki iliyopita. Ninatoa wito kwa makundi ya waasi kusitisha malumbano, na pande zote kuweka kando maslahi yao kwa muda mfupi na kutekeleza makubaliano ya amani."

Halikadhalika, amesema Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali(MINUSMA) ulioanzishwa miaka mitatu iliyopita umeimarishwa na baraza la usalama kusaaidia katika utekelezaji wa makubaliano ya amani, marejesho ya asasi za serikali, na kulinda raia.

Kwa mantiki hiyo Ban amesema MINUSMA inafanya kila liwezalo kusaidia kuleta utulivu katika maeneo ambapo kuna magaidi na ambapo askari wa Umoja wa mataifa wanakabiliwa na tishio la mlipuko wa mabomu, na hivyo...

(Sauti ya Ban)

"Katika mazingira haya hatari, MINUSMA bado inakabiliwa na upungufu wa rasilimali. Natoa wito kwa nchi wanachama kusaidia kwa haraka katika kuimarisha ujumbe huu."

Ban amezisihi nchi za Afrika Magharibi na Sahel kutoa mchango wao haraka, katika kukabiliana na tatizo la ukosefu wa amani katika ukanda huo, na kuimarisha ushirikiano wa mpakani kwa kupitia mikakati inayongozwa na Umoja wa Afrika, ECOWAS, G-5 Sahel na wengine.