Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mataifa nane yakwamisha utekelezaji wa CTBT, baraza lapitisha azimio kuzisihi

Mataifa nane yakwamisha utekelezaji wa CTBT, baraza lapitisha azimio kuzisihi

Miaka 20 tangu mkataba wa kupiga marufuku majaribio ya silaha za nyuklia, CTBT upitishwe, bado haujaanza kutekelezwa kutokana na mataifa nane yenye silaha hizo kutosaini na kuridhia mkataba huo.

Kufuatia hatua hiyo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limepitisha azimio ambalo pamoja na mambo mengine linataka nchi hizo kusaini na kuridhia ili mkataba uweze kuanza kutumika.

Nchi hizo nane ni pamoja na Misri ambayo leo wakati wa kupiga kura barazani haikuonyesha msimamo wowote huku wajumbe wengine 14 wakipitisha azimio hilo.

Mkataba huo ambao unataka nchi wanachama kutofanya majaribio ya nyuklia, ulianza kutiwa saini tarehe 24 Septemba mwaka 2006 na hadi sasa nchi 186 zimetia saini, huku 166 kati ya hizo zikiwa pia zimeridhia.

Hata hivyo hauwezi kuanza kutumika kwa kuwa bado mataifa manane kati ya 44 ambayo yana teknolojia ya nyuklia hayajatia saini na kuridhia.

Mataifa hayo ni Misri, China, Marekani, Korea Kaskazini, India, Iran, Israel na Pakistani.

Azimio limesisitiza kuwa mkataba huo ndio njia pekee ya kudhibiti nyuklia na kuimarisha amani na usalama duniani.