Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zerrrougui akaribisha kuachiliwa kwa watoto 21 Sudan Kusini

Zerrrougui akaribisha kuachiliwa kwa watoto 21 Sudan Kusini

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto na mapigano ya silaha, Leila Zerrougui, amekaribisha kuachiliwa huru kwa watoto 21 waliowekwa kizuizini na serikali ya Sudan kwa kujihusisha na makundi ya waasi.

Wavulana hao walisakwa wakati wa operesheni za kijeshi zilizofanywa katika jimbo la Darfur na wakawekwa kizuizini katika mji wa Khartoum tangu Aprili 2015. Mjumbe huyo maalum alikutana na watoto hao mwezi machi 2016 na akaanza kutetea kuachiliwa kwao.

Bi Zerrougui alisema anafurahi kuona kwamba watoto hao watapokea msaada kupitia mpango wa kuwaunganisha na jamii zao na pia kupata msamaha wa Rais. Mwezi machi, Sudan ilitia saini mkataba wa Umoja wa mataifa wa kukomesha matumizi ya watoto jeshini. Mpango huo unahusiana na kampeni iitwayo "watoto sio wanajeshi", unahimiza kusitisha ajira ya watoto jeshini.

Pia amepongeza ushirikiano mzuri kati ya Serikali ya Sudan na Umoja wa Mataifa katika kuunga mkono juhudi hizo.