Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan Kusini yatangaza mpango wa kurahisisha usambazaji misaada

Sudan Kusini yatangaza mpango wa kurahisisha usambazaji misaada

Serikali ya Sudan Kusini imekiri kuwa hali ya kibinadamu nchini humo ni mbaya na hivyo imetangaza mpango wake wa kurahisisha watoa huduma za kibinadamu kufanya kazi zao bila vikwazo vyovyote na kwa usalama.

Tangazo hilo limetolewa katika mkutano wa ngazi ya juu kuhusu hali ya kibinadamu nchini Sudan Kusini, mkutano uliofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Makamu wa kwanza wa Rais wa Sudan Kusini, Taban Deng Gai akihutubia mkutano huo amesema serikali imeagiza kuondolewa kwa vizuizi vyote visivyo halali na kukamata wahalifu wanaokwamisha usambazaji wa misaada na kwamba.

(Sauti ya Taban)

“Kuhusu nyaraka za usalama wa ndege, viza na vibali kuhusu ushuru, serikali na ofisi ya umoja wa mataifa ya kuratibu misaada wamekubaliana kuanzisha kituo kimoja huko UNMISS ili kushughulikia suala hilo. Hatua hii hili linalenga kuharakisha mchakato mzima wa kupata nyaraka zote zinazotakiwa.”

image
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akisisitiza umuhimu wa kulinda watoa huduma za kibinadamu. Picha: UN Photo/Laura Jarriel
Mapema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alisisitiza umuhimu wa kulinda watoa huduma za kibinadamu akisema kuwa tangu kuanza kwa mzozo wa Sudan Kusini mwezi Disemba mwaka 2013, wahudumu 63 wameuawa, huku wengine wakibakwa.

(Sauti ya Ban)

"Watoa huduma wanaweza kufanya kazi yao iwapo pande kwenye mzozo wataheshimu uhuru wao na iwapo wahisani waingilie kati wawasaidie. Hakuna suluhu la kijeshi kwenye mzozo huu zaidi ya janga na machungu makubwa kwa walio wachache.”