Skip to main content

WHO yazindua makakati wa kutokomeza magonjwa ya moyo

WHO yazindua makakati wa kutokomeza magonjwa ya moyo

Shirika la afya ulimwenguni WHO, leo  limezindua mkakati wa kukabiliana na magonjwa ya moyo  yakiwamo shambulio la moyo na kiharusi, magonjwa yanayoongoza kwa kusababisha vifo duniani.

Kwa mujibu wa WHO, zaidi ya watu milioni 17 hufariki dunia  kila mwaka  kutokana na magonjwa ya moyo, wengi wa wanaofariki hugundulika kutumia tumbaku, kula vyakula vyenye chumvi nyingi, na kutofanya mazoezi ambapo shirika hilo limesema wengi wanaweza kuokolewa kwa kupatiwa tiba za shinikizo la damu, shinikizo la lehemu  na mengine yanayosababisha magonjwa ya moyo na kiharusi.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dk Margaret Chan amenukuliwa akisema mkakati huo utaokoa maisha ya mamilioni ya watu kwa hatua za kuzuia magonjwa ya moyo katika jamii na katika nchi  ikiwamo kuweka ushuru katika tumbaku , kupunguza vyakula vyenye chumvi na tiba mujarabu.

Mkakati huo ni sehemu ya jitihada mpya ya kuongeza kinga na udhibiti wa magonjwa ya moyo hususani katika nchi zinazoendelea, ambapo kituo cha Marekani cha udhibiti wa magonjwa na kinga US CDC ma wadau wengine wa afya wanajumuishwa.