Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pande kinzani mjadili njia ya kuondokana na jinamizi la vita Syria:Ban

Pande kinzani mjadili njia ya kuondokana na jinamizi la vita Syria:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amezisihi leo pande za mzozo nchini Syria na nchi wanachama kujadiliana kwa haraka njia itakayo watoa watu wa Syria katika jahannamu.

Mzozo wa Syria wa miaka mitano umekatili maisha ya zaidi ya watu 300,000 na kusambaratisha wengine wengi. Juhudi za Umoja wa Mataifa hivi karibuni za kusitisha mapigano kwa muda, ili kupeleka msaada kwa waliokwama katika mapigano nchini humo iliishia kuwa hewa, baada ya msururu wa malori yaliyobeba msaada wa chakula, dawa na blanketi kushambuliwa hivi karibuni. Akizungumzia suala hilo katika kikao cha Baraza la Usalama leo, katibu mkuu Ban amesema...

(Sauti ya Ban)

"Natoa changamoto kwa kila mmoja wenu, kutumia ushawishi wenu wa haraka kusitisha mapigano, ili kuwezesha misaada ya kibinadamu, na kuunga mkono Umoja wa Mataifa katika kuchagiza mchakato wa kisiasa kwa ajili ya Wasyria, kujadili njia za jinsi ya kutoka katika jahannamu walikonaswa".

Naye Mwakilishi maalumu wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Bwana Staffan de Mistura ambaye pia alihutubia kikao hicho amesema, atawasilisha mfumo mpya kama kianzio cha mazungumzo kwa wadau wa mzozo, mfumo ambao utaunda mchakato wa kisiasa unaomilikiwa na kuongozwa na waSyria wenyewe, huku akisema..

(Sauti ya de Mistura)

"Mgogoro wa Syria hauwezi kutatuliwa kijeshi , na tunasema hili wakati wote lakini hatutekelezi, bali kwa njia ya mazungumzo ya kisiasa, inayomilikiwa na kuongozwa na waSyira wenyewe, baina ya Serikali na pande kinzani , ambapo watakubalina na kuridhia mfumo wenye kutekelezeka na utakaoleta mabadiliko ya kisiasa na kuunda katiba mpya na uchaguzi huru na wa haki chini ya usimamizi wa kimataifa."