Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yampa tuzo Rebecca kwa juhudi za kukomesha ndoa za utotoni Tanzania

UNICEF yampa tuzo Rebecca kwa juhudi za kukomesha ndoa za utotoni Tanzania

Na hatimaye, jitihada za kukomesha ndoa za utotoni nchini Tanzania zinazofanywa na mkurugenzi mtendaji  wa mpango uitwao Juhudi kwa msichana, Rebecca Gyumi zimetambuliwa na wadau wakiongozwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNCEF. Rosemary Musumba na taarifa kamili.

 (Taarifa ya Rosemary)

Rebecca amepewa tuzo na UNICEF za kutambua mchango wake katika hafla  maalum mjini New York iliyoandaliwa kwa pamoja na mpango jumuishi katika kutekeleza  maendeleo endelevu, Project Everyone, na shirika la kimataifa la bidhaa za vyakula na kujisafi Unilever.

Baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, binti huyo mwanaharakati amesema anaitoa mahususi kwa wasichana wote wa Tanzania na wengine kote duniani ambao wamehepa ndoa za utotoni na kusaka uhuru , akiongeza kuwa hao ndio wanaomhamasisha katika juhudi hizo.

Rebecca anayetajwa kuwa chachu ya ushindi wa kesi dhidi ya kibali cha ndoa za utotoni nchini Tanzania mwezi Julai ameiambia hadhira hiyo kuwa kubadilisha sheria ni hatua tu katika kuanikiza kampeni ya kukomesha kitendo hicho kilicho kinyume na utu.