Skip to main content

Sera ya sekta ya afya ya umma ni muhimu kutimiza SDG’s:Ban

Sera ya sekta ya afya ya umma ni muhimu kutimiza SDG’s:Ban

Kazi ya tume ya kimataifa ya ajira ya afya na ukuaji wa uchumi ni muhimu sana katika kufanikisha ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu yaani SDG’s na kutimiza ahadi ya kutomwacha yeyote nyuma.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa katika taarifa yake kwenye kikao cha ngazi ya juu cha tume hiyo, taarifa iliyosomwa kwa niaba yake na mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani Bi Margaret Chan.

Taarifa hiyo inasema idadi ya watu duniani sio tu kwamba inaongezeka bali pia inazeeka, hasa kutokana na kupanda kwa hali ya maisha.

Ban amesema tatizo kubwa katika azima hii ni magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama kisukari na saratani yanayoathiri watu wengi zaidi kuliko wakati mwingine wowote, huku ikikadiriwa kwamba ifikapo 2030 mahitaji ya huduma ya afya yatazalisha ajira milioni 40 duniani kote.

Hata hivyo amesema asilimia kubwa ya ajira hizo zitakuwa kwenye nchi tajiri, na bado kutakuwa na upungufu wa wahudumu wa afya milioni 18 kote duniani huku waathirika wakubwa wakiwa nchi zinazoendelea.