Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio la Aleppo halikubaliki na linalaaniwa:UM

Shambulio la Aleppo halikubaliki na linalaaniwa:UM

Leo Umoja wa Mataifa umeshtushwa na kulaani vikali shambulio la msafara wa misaada kwa ajili ya watu 78,000 walionaswa katika mapigano Kaskazini-Mashariki mwa Aleppo nchini Syria. Shambulio hilo la Jumatatu usiku, limekatili maisha ya mfanyakazi mmoja wa masuala ya kibinadamu na watu wengine wengi wasiojulikana.

Msafara huo uliowezeshwa na muungano wa Umoja wa Mataifa pamoja na Shirika la Hilali Nyekundu la Syria(SARC), ulikuwa umebeba chakula, vifaa vya matibabu, na mablanketi. Mazungumzo ya kusitisha mapigano kwa muda kutoa misaada yamekuwa yakiendelea, na kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa msafara huu ulipata ruhusa hiyo.

Jans Laerke ni msemaji wa Shirika la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA, Geneva....

(Sauti ya Jans)

"Siku hii, imegubikwa na kiza na huzuni kwa watoaji msaada Syria na nafikiri dunia nzima, kwa sababu nadhani kumekuwa na mshituko na kwa kweli kuchukizwa sana na shambulio hili. Tunasimama kidete na bila kutikiswa na kwa kadri ya uwezo wetu, kusaidia watu wa Syria wenye mahitaji."

Nayo Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) imesema itafanya uchunguzi na kuwafikisha wahusika mbele ya sheria.