Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ugaidi ni tishio kubwa la karne hii: Rais wa Chad

Ugaidi ni tishio kubwa la karne hii: Rais wa Chad

Ugaidi umeelezwa kama tishio la karne kwa afrika, na Rais wa Chad alipohutubia mjadala wa 71 wa baraza kuu la Umoja wa mataifa Jumanne.

Makundi yenye itikadi kali likiwemo kundi la Boko Haram yameathiri saana eneo la bonde la ziwa Chad na kusababisha janga la kibinadamu.

Umoja wa mataifa unasema kuna watu zaidi ya milioni tisa kwenye bonde la ziwa Chad ambao wanahitaji msaada wa kibinadamu, huku mtu mmoja kati ya watatu anakabiliwa matatizo ya uhakika wa chakula katika maeneo yaliyoathirika na machafuko ya Boko Haram.

Rais Idriss Deby akizungumza kupitia mkalimani ameonya kwamba ugaidi unaweza kusambaa Afrika.

(SAUTI YA RAIS DEBY)

"Afrika leo hii inabeba gharama kubwa za ugaidi, tishio la karne. Somalia, Libya, Mali, bonde la ziwa Chad, na eneozima la Sahel , limearithirika vibaya na hatari inatishia kusambaa katika bara zima.”

Umoja wa Mataifa unaendelea kuisaidia Chad. Wiki iliyopita mratibu wa Umoja wa mataifa wa masuala ya kibinadamu Stephen O’Brien alidhinisha kutengwa dola milioni 10 kutoka fuko la kimataifa la misaada ya dharura CERF kusaidia operesheni za kibinadamu Chad.