Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua zichukuliwe kufuatia ukiukwaji mkubwa wa haki Burundi:Ripoti

Hatua zichukuliwe kufuatia ukiukwaji mkubwa wa haki Burundi:Ripoti

Ripoti ya mwisho ya tume huru ya Umoja wa Mataifa ya uchunguzi nchini Burundi imechapishwa leo Jumanne, ikieleza ushahidi wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Ripoti inasema ukiukwaji huo una uwezekano wa kuwa ni uhalifu dhidi ya ubinadamu uliotekelezwa na serikali ya Burundi na watu wanaohusika na serikali.Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Kutokana na matokeo ya uchunguzi yanayodhihirisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, historia ya machafuko ya kikabila ya nchi hiyo, ukwepaji sheria na hatari ya kusambaa kwa ghasia, wataalamu wameitaka serikali ya Burundi, Muungano wa Afrika, Baraza la haki za binadamu, Baraza la usalama na wadau wengine wa kimataifa, kuchukua hatua madhubuti ili kulinda mkataba wa Arusha wa 2005, ambao ulipelekea kuwa na amani ya muda mrefu Burundi tangu taifa hilo lipate uhuru.

Hatua hizo ni pamoja na kuundwa tume ya kimataifa ya uchunguzi, kushirikisha mchakato huru wa kimataifa wa kisheria, kufikiria upya uanachama wa Burundi kwenye baraza la haki za binadamu na utekelezaji wa kifungu nambari VII cha mkataba wa Umoja wa Mataifa endapo Burundi itaendelea kutotimiza maazimio ya Umoja wa Mataifa.