Skip to main content

Kuhama lazima iwe kitendo cha uchaguzi - FAO

Kuhama lazima iwe kitendo cha uchaguzi - FAO

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la chakula na kilimo duniani FAO, José Graziano da Silva amesema hii leo kuwa kuhama kwa watu kutoka makwao kiwe kitendo cha kuchagua badala ya lazima.

Akizungumza kwenye kikao cha ngazi ya juu kuhusu wakimbizi na wahamiaji Bwana da Silva amesema ili hilo lifanikiwe ni vyema kuimarisha fursa za kuwaruhusu watu vijijini kuepuka kuhama makwao kutokana na shinikizo.

Ametaja hatua ya kwanza iwe ni kushughulikia mambo ambayo husababisha watu kuhama kwa dhiki na pia juhudi za pamoja zifanywe ili kuleta kilimo endelevu na maendeleo katika vijiji kama sehemu muhimu ya ufumbuzi wowote na kuwezesha watu hao kubaki makwao.

Akiongezea mkurugenzi huo alisema kuwa kumekuwa na kiasi kikubwa cha harakati za mpakani katika miaka ya hivi karibuni ambazo zimezua mvutano katika baadhi ya nchi, na kusababisha kuweka suala la uhamiaji ajenda ya juu kwenye masuala ya diplomasia.

Akitaja kuwa tangu zama za kale uhamiaji ukiendelea kwa ajili ya maendeleo, lakini sasa gharama inakuwa kubwa mno wakati huu ambapo watu wanaona hawana namna bali kuacha makazi yao na kusaka maisha kwingineko.