Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji ni jasiri lakini bado wanakumbwa na hatari- Sutherland

Wahamiaji ni jasiri lakini bado wanakumbwa na hatari- Sutherland

Kujumuishwa kwa shirika la kimataifa la uhamiaji, IOM ndani ya Umoja wa Mataifa, ni ishara ya umoja huo kuimarisha majukumu yake ya kushughulikia masuala ya uhamiaji.

Hiyo ni kauli ya Peter Sutherland, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliyotoa baada ya kutiwa saini kwa makubaliano ya shirika hilo sasa kutambuliwa kuwa ni shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa.

Amesema hatua hiyo imekuja wakati muafaka ili kusaidia wahamiaji ambao amesema ni majasiri lakini pia wako hatarini zaidi.

Bwana Sutherland amesema hatua hiyo sambamba na ile ya azimio la New York, litaondoa dhana iliyozoeleka ya nchi kutowajibika kusaidia wahamiaji na badala yake kuachia jukumu zima kwa nchi iliyo karibu zaidi na janga linalosababisha wakimbizi.

Amesema hivi karibuni atachapisha ripoti yake inayolenga kuwezesha kushughulikia suala la wahamiaji kwa njia bora zaidi na kwa pamoja zaidi.