Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ombi la UNHCR #WithRefugees kukabidhiwa Katibu Mkuu UM

Ombi la UNHCR #WithRefugees kukabidhiwa Katibu Mkuu UM

Zaidi ya watu milioni 1 nukta Tatu wameweka saini kwenye ombi la kuonyesha mshikamano na wakimbizi, litakalokabidhiwa hii leo kwa Katibu Mkuu wa Umoja Ban Ki-moon na Rais wa Baraza Kuu la umoja huo Peter Thomson mjini New York, Marekani. Rosemary Musumba na ripoti kamili.

(Taarifa ya Rosemary)

Filippo Grandi, Kamishna mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na wakimbizi, UNHCR, amewashukuru mamilioni ya watu walioweka saini zao kwenye ombi hilo ili kuonyesha mshikamano wao na mamilioni ya wakimbizi.

Akizungumzia juu ya ombi hilo lililozinduliwa mwezi Juni mwaka huu, Bwana Grandi amesema kuwa migogoro na mitikisiko imeongezeka zaidi wakati huu na kusababisha watu wengi zaidi kukimbia makazi yao.

Amesema kila mtu ajihusishe ili kusaka majibu ya kweli kwa hatma ya wakimbizi akieleza kuwa ombi hilo linaweka bayaan changamoto za nyakati za sasa.

Ombi hilo lina simulizi kadhaa ikiwemo za mtoto mkimbizi Alan Kurdi aliyefariki dunia wakati wa kusaka hifadhi ulaya.