Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makundi ya kiraia ni muhimu katika demokrasia ya kufanikisha SDGs- Ban

Makundi ya kiraia ni muhimu katika demokrasia ya kufanikisha SDGs- Ban

Misingi ya demokrasia imejikita katika kila lengo la maendeleo endelevu SDGs ikitaka kuwepo na jamii shirikishi na taasisi zinazowajibika.

Ni sehemu ya ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon katika siku ya kimataifa ya demokrasia hii leo.

Ban amesema malengo hayo kuanzia huduma za umma, afya hadi elimu yanaonyesha jinsi utawala wa kidemokrasia unavyoweza kuboresha ustawi wa watu na maendeleo ya kibinadamu.

Kwa mantiki hiyo amesema wakati huu ambapo ajenda hiyo ya 2030 inapolenga kuhakikisha hakuna mtu yeyote anayesahaulika, ni vyema kuhakikisha kuwa utekelezaji unajumuisha makundi ya kiraia yaliyo thabiti na kutoka pande zote hata yale ya pembezoni.

Amesema ni vyema kulinda uhuru wa makundi ya kiraia kufanya kazi zao muhimu.

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa katika kuadhimisha siku hii umetoa video inayobainisha nafasi ya demokrasia katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu ili hatimaye dunia iwe kitu kimoja na ustawi bora mmoja.