Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la UM waanza rasmi leo

Mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la UM waanza rasmi leo

Hii leo Rais wa mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Peter Thomson kutoka Fiji amekula rasmi kiapo cha kuongoza chombo  hicho kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kuanza kwa mkutano huo kulitanguliwa na taratibu za makabidhiano kutoka kwa Rais wa mkutano wa 70 Mogens Lykketoft..

Nats..

Baada ya kutangaza rasmi kufungwa kwa mkutano wa 70 ndipo Bwana Mogens alipomkabidhi rasmi Bwana Thomson, rungu la kuongoza vikao hivyo, naye akaitisha kikao cha kwanza kinachozungumzia kanuni za uendeshaji.

Awali kabla ya kula kiapo Bwana Thomson alitangaza kuwa maudhui ya mkutano huo wa 71 ni Maendeleo endelevu;msukumo wa kimataifa ili kubadili dunia.

Na katika kuweka msisitizo hasa katika kufanikisha malengo hayo 17 aliwaita jukwaani wajukuu zake wawili mmoja akiwa na umri wa miaka Saba na mwingine mitano akisema ukomo wa ajenda 2030, watakuwa ni vijana.

image
Rais wa Baraza Kuu la UM Peter Thomson akiwa na wajukuu zake. (Picha:WebTv Video capture)
Hivyo akahoji je itakuwa dunia ambayo athari za mabadiliko ya tabianchi zitashindwa kudhibitiwa au umaskini utasababisha ghasia na uhamiaji?

Amesema iwapo utashi wa ubinadamu ni thabiti vya kutosha, mwaka 2030 itakuwa dunia ambamo kwayo nishati inatosha na kila mtu anaweza kuipata na wanawake na wanaume watakuwa na ajira zenye hadhi hivyo akasema..

(Sauti ya Thomson)

“Ni wazi kuwa ni mwelekeo wa dunia bora ambayo tunapaswa kuelekea na naapa kwa mapendo yangu kwa wajukuu zangu, kuwa nitafanya kila niwezalo ndani ya mamlaka yangu ya Rais wa mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kusongesha ajenda ya maendeleo endelevu na kuahidi  mwelekeo wa maisha endelevu kwenye sayari hii utafanikiwa mwaka 2030 utakapofika.”

Baada ya kikao, Rais huyo wa mkutano wa 71 alizungumza na wanahabari ambapo alizungumzia masuala kadhaa ikiwemo timu aliyounda kusongesha malengo ya maendeleo endelevu.

image
Rais wa Baraza Kuu la UM Peter Thomson akizungumza na wanahabari. (Picha:WebTV video capture)