Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Majukumu ya ujumbe wa UM Colombia yawekwa bayana

Majukumu ya ujumbe wa UM Colombia yawekwa bayana

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo kwa kauli moja limepitisha azimio linalobainisha ukubwa na majukumu ya utendaji ya ujumbe wa umoja huo nchini Colombia ulioanzishwa mwezi Januari mwaka huu.

Ujumbe huo uliundwa kufuatia ombi la serikali ya Colombia la kutaka Umoja wa Mataifa usaidie katika kusimamia utekelezaji wa mkataba wa amani kati ya serikali na kikundi cha waasi cha  FARC-EP.

Azimio hilo linaeleza kuwa ujumbe huo utakuaw na watendaji raia 450 ambao watakuwa waangalizi kwenye ukanda wa kufuatilia kuwa hakuna mapigano tena pamoja na usalimishaji wa silaha.

Waangalizi hao watafuatilia na kuthibisha kuwa mkataba huo wa kusitisha mapigano unazingatiwa na ufuatiliaji huo wa pande tatu unahusisha Umoja wa Mataifa, serikali ya Colombia na kikundi cha FARC-EP.

Mwakilishi wa kudumu wa Venezuela kwenye Umoja wa Mataifa balozi Rafael Ramirez amesema azimio hilo ni jambo la msingi katika hatua ya jamii ya kimataifa ya kufuatilia na kuthibitisha utekelezaji wa mkataba huo alioita wa kihistoria.

"Kwa hiyo basi kuna umuhimu wa Umoja wa Mataifa kushiriki kwa mapana yote, siyo tu katika kutoa fedha kuwezesha ujumbe wake Colombia, lakini muhimu kuziba vyanzo vya mzozo na kuweka fursa za kisiasa na kiuchumi kwa waliokuwa wapiganaji na usaidizi wao kwenye mchakato wa kisiasa.”

Wajumbe wa baraza hilo wamesema wameunga mkono azimio hilo kuonyesha azma ya jamii ya kimataifa ya kujenga amani Colombia baada ya mzozo huo wa zaidi ya miaka 50.