Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama na DPRK

Baraza la Usalama na DPRK

Kufuatia kitendo cha Korea Kaskazini kufanya jaribio la nyuklia chini ya ardhi siku ya Ijumaa, wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamekubaliana kuanza kuchukua mara moja hatua stahiki kwa mujibu wa ibara ya 41 ya azimio namba 2270 ya baraza hilo kuhusu nchi hiyo.

Ibara hiyo inatoa wito kwa nchi kupatia taarifa zozote baraza hilo kuhusiana na ukiukwaji wa hatua zilizotangazwa kwenye maazimio tangulizi namba 1718 (2006), 1874 (2009), 2087 (2013), 2094 (2013) au azimio namba 2270.

Hatua hizo zinazoangaliwa iwapo zinakiukwa ni pamoja na vikwazo vya kifedha vinavyoweka kiwango cha shughuli za kibenki za DPRK nje ya nchi hiyo na zuio la safari na mali kwa baadhi ya watendaji.

Akisoma taarifa ya wajumbe hao mbele ya wanahabari, baada ya kikao chao cha faragha, Rais wa baraza hilo kwa mwezi huu wa Septemba Balozi Gerard Van Bohemen wa New Zealand amesema pamoja na kutoa msimamo huo, wajumbe wamelaani wakisema ni kitendo kisicho na haya cha kupuuza maazimio na mikataba ya kimataifa.