Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OCHA: Dola milioni 7 zatolewa kwa misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi wa ndani Somali

OCHA: Dola milioni 7 zatolewa kwa misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi wa ndani Somali

Mratibu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Peter de Clercq ametoa msaada wa dola milion 7 hapo tarehe 26 Agosti ili kuongezea mfuko wa wahisani mbali mbali kusaidia nchi hiyo kuweza kuokoa maisha na kuimarisha huduma za ulinzi kwa watu waliokimbia makazi yao mjini Mogadishu.

Huu ni mgao wa pili ili kusaidia watu waliokimbia makazi yao mwaka huu, na utasaidia pia elimu, uhakika wa chakula, afya, lishe, ulinzi, malazi na maji na shughuli za usafi wa mazingira katika kambi ya Daynille na Kaxda zilizo karibu Mogadishu. Kambi hizi mbili zimekuwa wenyeji wa zaidi ya watu 120,000 waliokimbia makazi yao baada ya kuondolewa kwa nguvu kutoka maeneo mengine ya mji wa Mogadishu mwaka 2015.

Hali ya maisha katika makazi haya ni ya kusikitisha, huduma za jamii ni mdogo au hazipo, na ukiukwaji wa haki za binadamu ni tatizo kubwa. Mgao wa kwanza wa dola milioni 7 ulitolewa mwezi Julai kwa watu waliokimbia makazi yao huko Baidoa na Kismayo.

Mratibu huyo amesema wakimbizi wa ndani nchini Somalia wanakabiliwa na changamoto kubwa sana, na umakini wa msaada wa kibinadamu na kwa wakati ni muhimu ili kushughulikia mahitaji yao kwa haraka. Ameongeza kuwa wanaotoa misaada na nia yao ni kupunguza mateso ya watu wasio na makazi, kutoa misaada ya kujikimu kimaisha na kuendeleza juhudi za maendeleo kwa lengo la kupunguza watu kukimbia makazi yao kwa muda mrefu nchini Somalia