Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nasikitika namaliza n'gwe yangu DPRK ikiendelea na majaribio ya nyuklia- Ban

Nasikitika namaliza n'gwe yangu DPRK ikiendelea na majaribio ya nyuklia- Ban

Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-moon akizungumza na wanahabari- (Picha:WebTv Video capture)Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema anasikitishwa sana kuwa jitihada zake za kuhakikisha Korea Kaskazini inaachana na mpango wa nyuklia hazikufanikiwa katika kipindi chake cha miaka 10 wakati huu ambapo kinafikia ukingoni.

Amesema hayo wakati akijibu swali la waandishi wa habari mjini New York, Marekani aliozungumza nao kuelezea masikitiko yake ya jaribio la leo la nyuklia liliofanyika chini ya ardhi huko Korea Kaskazini ijulikanayo pia kama Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea.

“Nimekuwa najaribu kwa kadri ya uwezo wangu kama Katibu Mkuu kuboresha chochote kinachowezekana katika miaka hii 10 ya uongozi wangu, lakini  nasikitisha kuwa sijaweza kufanikisha matarajio yangu yote au ya jamii ya kimataifa. Na nitaendelea kufanya  hivyo hadi nimalize ng’we yangu. Lakini kwa kweli kabisa nia yangu na mipango yangu haikufanika kutokana na hali hii inayobadilika huko rasi ya Korea.”

image
Awali Ban alilaani vikali jaribio hilo, la tano ndani ya miaka 10 akisema…

“Nalaani vikali jaribio hilo la nyuklia lilikofanywa na Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK. Huu ni ukiukwaji usio na haya wa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.”

Hivyo akatoa wito ..

“Natoa wito kwa jamii ya kimataifa iungane na kuisihi DPRK ibadili mwelekeo wake na kuazimia kuachana na nyuklia. Baadala ya kutumia silaha za nyuklia na teknolojia ya makombora ya masafa marefu, DPRK inapaswa kuendeleza maisha  bora ya wananchi wake.”

Amelisihi Baraza la Usalama kusalia na mshikamano kwenye suala hilo na kuchukua hatua sahihi huku akisema..

“Tunafuatilia na kutathmini yanayoendelea baada ya jaribio hili la nyuklia kwa ushirikiano wa karibu na mashirika husika ya kimataifa, ikiwemo lile la mkataba wa kupinga marufuku majaribio ya nyuklia na pande zenye maslahi na suala hilo.”