Skip to main content

Michezo ya olimpiki ya watu wenye ulemavu yang'oa nanga Rio

Michezo ya olimpiki ya watu wenye ulemavu yang'oa nanga Rio

Hii leo michezo ya olimpiki kwa watu wenye ulemavu imeng’oa nanga huko Rio de Janeiro nchini Brazili, ufunguzi ulioenda sambamba na uzinduzi wa video mpya inayoonyesha ushirikiano kati ya wachezaji kandanda wa klabu ya Barcelona na timu ya taifa ya Hispania ya watu wenye ulemavu wa kutoona.

Video hiyo inaonyesha wachezaji watano wa FC Barcelona wakicheza wakiwa wamezibwa macho wakichuana na timu hiyo, ambao video imeandaliwa ili kuonyesha fursa ya michezo katika kuleta usawa kwa kila mtu.

Waandaaji wa video hiyo ni shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, klabu ya Barcelona na kamati ya kimataifa ya watu wenye ulemavu, IPC na itaendelea kuonyeshwa katika kumbi mbali mbali huko Rio hadi tarehe 18 mwezi huu.

Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Anthony Lake amesema michezo ya watu wenye ulemavu inathibitisha kwamba uwezo, nasio ulemavu, ndio unaokamilisha kile ambacho binadamu anaweza kutimiza  katika maisha.

image
Mpira uliotumika kwenye mechi hiyo ambapo unatoa sauti ili wachezaji wenye ulemavu wa kutoona waweze kufuatilia na kucheza. (Picha:Unifeed/Video capture)
Amesema UNICEF inafurahia kuungana pamoja na timu ya Barçelona kuwapatia watoto wengi zaidi nafasi ya kucheza, kujifunza na kufanya mengi kadri ya uwezo wao, akisema kuwa hivyo ndivyo maisha ya utoto yalivyo.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekaribisha kuanza kwa michezo ya olimpiki ya walemavu huko mjini Rio de Janeiro.

Msemaji wa Katibu mkuu, Stephane Dujarric amemnukuu Ban akisema kuwa anaamini kwamba michezo ina njia muhimu hasa kwa kukuza na kutekeleza mkataba wa haki za watu wenye ulemavu.

Katibu Mkuu amesema anaamini kuwa wanariadha wenye walemavu wanatoa mfano wa kuigwa na ni ishara ya ujasiri kwa kila mtu.