Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujumbe wa Afrika waelekea Gabon kusaka suluhu baada ya uchaguzi

Ujumbe wa Afrika waelekea Gabon kusaka suluhu baada ya uchaguzi

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika ya Kati, UNOCA, Abdoulaye Bathily atawakilisha umoja huo kwenye ujumbe wa ngazi ya juu unaongozwa na Afrika huko Libreville, Gabon.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amewaambia wanahabari kuwa ziara hiyo inayofanyika kwa muktadha wa Afrika, ni sehemu ya juhudi za bara hilo kusaka ufumbuzi wa kudumu wa mzozo ulioibuka baada ya uchaguzi mkuu nchini Gabon na kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa rais tarehe 27 mwezi uliopita.

Katika juhudi zake, Bathily anaendelea kuhamasisha wadau wote kutumia njia za kisheria zilizopo ili kusuluhisha  migogoro baina yao.

Na katika muktadha huo hivi karibuni alimtembelea kiongozi wa upinzani Jean Ping huku ikielezwa kuwa Bwana Bathily anaendelea kuwasiliana na Rais Ali Bongo Ondimba.

Tarehe ya mwisho ya kuwasilisha rufaa kwa mahakama ya Katiba dhidi ya uchaguzi ni tarehe  Nane Septemba mwaka huu saa kumi jioni.