Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki za binadamu kuangaziwa Sudan Kusini

Haki za binadamu kuangaziwa Sudan Kusini

Tume ya Umoja wa Mataifa ya  haki za binadamu huko Sudan Kusini leo inaanza ziara ya siku 19 nchini humo, ziara ambayo itawapeleka hadi Uganda na Ethiopia. Amina Hassan na maelezo kamili.

(Taarifa ya Amina)

Wakati wa ziara hiyo, makamishna watatu wanaounda tume hiyo, Yasmin Sooka, Ken Scott na Godfrey Musila, watakuwa na vikao na viongozi wa kisiasa, wakimbizi, wakimbizi wa ndani na mashirika ya kimataifa kwa lengo la kuangazia haki za binadamu Sudan Kusini.

Miongoni mwa viongozi hao ni Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, na watakwenda hadi vituo vya kuhifadhi wakimbizi wa ndani huko Juba na Bentiu.

Kutoka Sudan Kusini wataelekea Addis Ababa, Ethiopia kukutana na viongozi wa muungano wa Afrika na hatimye Uganda kwenye kambi ya Adjumani ambako kuna makazi ya kuhifadhi wakimbizi wa Sudan Kusini.

Tume hiyo iliundwa mwezi machi mwaka hu na baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa, ambao ina jukumu la kufuatilia na kuripoti kuhusu haki za binadamu Sudan Kusini, kuweka misingi ya haki na kutoa mwongozo wa masuala ya haki kwa serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa.

Ripoti ya ziara yao itawasilishwa mbele ya baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mwezi Machi mwakani.