Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yataja washindi wa tuzo ya Nansen 2016

UNHCR yataja washindi wa tuzo ya Nansen 2016

Tuzo ya mwaka huu ya Nansen inayotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi imekwenda kwa wafanyakazi wa kujitolea raia wawili wa Ugiriki, Konstantinos Mitragas na Efi Latsoudi.

Tuzo hiyo inayolenga watu au vikundi vinavyosaidia kuboresha maisha ya wakimbizi imenyakuliwa kwa pamoja na Mitragas kutoka shirika lisilo la kiserikali la uokoaji baharini, Hellenic Rescue Team ilhali Latsoudi anatoka kijiji cha PIKPA huko kisiwani Lesvos.

Wawili hao walijitoa kwa hali na mali kuokoa wakimbizi kwenye fukwe za Ugiriki wakati wa janga la wakimbizi mwaka jana na vile ambavyo wao na jamii zao walikaribisha wakimbizi.

Zaidi ya watu 850,000 waliwasili nchini Ugiriki kwa njia ya bahari mwaka jana mabapo zaidi ya 500,000 kati yao waliingilia kisiwa cha Lesvos.

Akizungumza kuhusu uteuzi wa wawili hao Kamishna mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi amewasifu washindai hao akisema shirika la Hellenic pamoja na Latsoudi walikataa kuwa watazamaji wa janga hilo na badala yake walijitokeza kusaidia.