Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia zikizidi Syria, wananchi wakata tamaa- Wachunguzi

Ghasia zikizidi Syria, wananchi wakata tamaa- Wachunguzi

Kadri ghasia na mapigano yanavyozidi nchini Syria, kasi ya wananchi ya kukata tamaa inazidi kuongezeka, wamesema wachunguzi wa Umoja wa Mataifa katika ripoti yao waliyotoa leo huko Geneva, Uswisi mbele ya wanahabari.

Mwenyekiti wa tume hiyo ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa, Paulo Pinheiro amesema katika janga hilo la zaidi ya miaka mitano sasa, pande zote kwenye mzozo zinashambulia raia  tangu kusambaratika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano mwezi Februari mwaka huu.

Bwana Pinhero akagusia sitisho la mapigano la hivi karibuni akisema..

“Sitisho la mapigano kwa muda mfupi limeonyesha ni kwa jinsi gani palipo na utashi wa kisiasa ndani ya jamii ya kimataifa na ndani ya Syria kwenyewe, unaweza kupunguza kwa haraka machungu wanayopata raia, lakini kama unavyofahamu sitisho hilo halikudumu muda mrefu.”

Kwa mujibu wa ripoti yao ya leo, ghasia na mapigano vimefikia kiwango kisicho cha kawaida huko mashariki mwa Aleppo ambako raia hawawezi kukimbia mashambulio ya kila uchao.