Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Timu ya wakimbizi katika mashindano ya wenye ulemavu Rio

Timu ya wakimbizi katika mashindano ya wenye ulemavu Rio

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa kwa Wakimbizi nchini Brazil, Isabel Marquez,  anakutana  hii leo na wanariadha wakimbizi wenye ulemavu wanaoshiriki mashindano ya olimpiki yanayong’oa nanga kesho.

Wanamichezo hao ni Ibrahim al Hussein kutoka Syria ambaye anashiriki mashindano ya kuogelea katika  mita 50 na mita 100 na Shahrad Nasajpour kutoka Iran ambaye anashindana katika mchezo wa kurusha kitufe.

Mwakilishi huyo atachukua fursa hiyo kuwatia moyo na kuwapongeza wanariadha hao kwa fursa ya kushiriki katika michezo hiyo ya Olympiki kwani wanawakilisha maelfu ya wakimbizi na wasaka hifadhi wengine duniani.

Bi. Marquez amesema wanariadha hao wameonyesha ujasiri na uvumilivu wa wakimbizi na pia watu wanaokimbia makazi yao,  idadi ambayo kwa sasa inazidi milion 65 kote ulimwenguni.