Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfumo wa elimu ubadilike ili ukidhi ajenda 2030- Ripoti

Mfumo wa elimu ubadilike ili ukidhi ajenda 2030- Ripoti

Ripoti mpya ya ufuatiliaji wa elimu duniani, inaonyesha kuwa mfumo wa elimu unahitaji mabadiliko makubwa ili uweze kuchochea utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Ikipatiwa jina la “Elimu kwa binadamu na sayari”,  ripoti hiyo iliyoandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO inasema kwa mwelekeo wa sasa elimu ya msingi kwa wote itafikiwa mwaka 2042, ile ya sekondari ya chini mwaka 2059 ilhali ile ya sekondari ya juu mwaka 2084.

Mkurugenzi Mkuu wa  UNESCO Irina Bokova amesema hiyo ina maana kuwa ifikapo mwaka 2030, ambao ni ukomo wa ajenda 2030, dunia itakuwa imefikia nusu ya utekelezaji hivyo mabadiliko ya msingi yanatakiwa kwenye mtazamo wa elimu, ikiwemo stadi sahihi ili kufanikisha maendeleo endelevu na shirikishi.

Amesema mfumo wa elimu unapaswa kuhakikisha watu wanapata stadi na ufahamu sahihi vinavyowawezesha kuwa na viwanda visivyoharibu mazingira na kupata suluhu za uharibifu wa mazingira.

Ripoti hiyo inataka serikali ikiwemo zile za Afrika kuanza kushughulikia ukosefu wa usawa kwenye sekta ya elimu kwa kupata taarifa sahihi kuanzia ngazi ya kaya.