Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tutahakikisha wanawake wanashiriki vyema kwenye uchaguzi Somalia-UNSOM

Tutahakikisha wanawake wanashiriki vyema kwenye uchaguzi Somalia-UNSOM

Nchini Somalia, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa, Michael Keating amesema atahakikisha wanawake wanashiriki ipasavyo kwenye uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu. Taarifa zaidi na John Kibego.

(Taarifa ya Kibego)

Amesema hayo wakati wa mkutano kati yake na wanawake mashuhuri wakiongozwa na Waziri wa masuala ya wanawake na haki za binadamu Zahra Samatar.

Katika mkutano huo, wanawake hao walieleza wasiwasi wao kuwa viongozi wa kisiasa katika jukwaa la uongozi la kitaifa, bado hawajaridhia mikakati mahsusi ya kutekeleza mapendekezo ya kuwa na asilimia 30 ya viti vya wabunge wanawake watakaotokana na uchaguzi huo.

Mathalani Bi. Samatar alisema walipatiwa jukumu la kuandaa kamati ya mapitio kushughulikia kutokuwepo kwa wanawake kwenye siasa lakini inavyoonekana ni kwamba jamii imeshawishiwa ione kuwa hoja ya ushiriki wa wanawake ni ya shinikizo.

Kufuatia hoja hiyo, Bwana Keating amesema Umoja wa Mataifa utashirikiana na viongozi wa Somalia ili kuona umuhimu wa kuendeleza ushiriki wa wanawake katika mchakato huo wa uchaguzi.