Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kaa chonjo na wanasiasa wanaosaka umaarufu mitandaoni- Zeid

Kaa chonjo na wanasiasa wanaosaka umaarufu mitandaoni- Zeid

Kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein amesema baadhi ya wanasiasa nchini Marekani na Ulaya wanaotumia kauli za kusaka umaarufu kwa maslahi yao badala ya kusaka ukweli wanaweza kuibua ghasia na hofu miongoni mwa jamii.

Akihutubia huko The Hague, Uholanzi, Zeid amemtaja mwanasiasa Geert Wilders wa Uholanzi  ambaye hivi karibuni amechapisha ilani ya uchaguzi ya chama chake ambapo yaelezwa kuwa anapendekeza kufungwa kwa misikiti yote nchini Uholanzi na kupiga marufuku kurani tukufu.

Kamishna Zeid amesema Wilders kama walivyo wanasiasa wengine kama vile Donald Trump wa Marekani, Marine Le Pen wa Ufaransa na Nigel Farage wa Uingereza hawana tofauti na kikundi cha ISIS au Da’esh

Amesema wanasiasa wa aina hiyo hawasemi ukweli kamilifu wa jambo fulani na badala yake wanarahasisha kauli zao za kisiasa kupitia mitandao ya kijamii huku wakijaribu kupunguza uwezo wa fikra za watu kwa kuweka nukuu fupi zisizo na maelezo ya kutosha.

“Hebu msichukue ndivyo sivyo. Bilas haka silinganishi vitendo vya wanasiasa hao wanaosaka umaarufu kwa kauli za hila na vitendo vya ISIS au Da’esh ambavyo vinachosha na ni vya kikatili. Da’eshi lazima wafikishwe mbele ya sheria. Lakini mbinu zao za mawasiliano, matmizi yake ya ukweli usio kamilifu na kurahisisha mambo, na propaganda za Da’esh ni sawa na za wasaka umaarufu. Na pande zote za mfumo huu zinanufaishana na haziwezi kupanua wigo wao bila ya vitendo vya mwenzake.”

Kamishna Zeid ametaja wanasiasa hao wa Marekani na Ulaya akisema kuwa hila zao na ghilba si sahihi katika zama za sasa kwani kauli zao zinaweza kuondoa stahmala miongoni mwa jamii.