Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan Kusini yaridhia kikosi cha kikanda

Sudan Kusini yaridhia kikosi cha kikanda

Hatimaye serikali ya Sudan Kusini imeridhia kupelekwa kwa kikosi cha kikanda cha askari 4,000 kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa raia, kikosi ambacho kimepatiwa mamlaka na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hivi karibuni.

Tangazo la kukubaliwa kwa kikosi hicho limekuja wakati wa ziara ya siku tatu ya wajumbe wa baraza hilo nchini Sudan Kusini matarajio yakiwa ni kwamba kikosi hicho kitaimarisha usalama na hivyo wananchi kuweza kurejea makwao.

Martin Elia Lomuro, waziri katika serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa alisoma taarifa ya pamoja baada ya wajumbe wa baraza hilo kukutana na Rais Salva Kiir mjini Juba.

“Umoja wa Mataifa na serikali ya mpito ya Umoja wa kitaifa wakubaliana kushirikiana katika ari mpya ili kusongesha maslahi ya wananchi wa Sudan Kusini. Wamekubaliana kuwa mahitaji ya kibinadamu na kiusalama ndio kipaumbele. Ili kuimarisha usalama, serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa imeridhia kupelekwa kwa kikosi cha ulinzi wa kikanda kama sehemu ya UNMISS.”