Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Marekani na China zaridhia mkataba wa Paris

Marekani na China zaridhia mkataba wa Paris

China na Marekani zimewasilisha nyaraka za kukubali na kuridhia mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi uliopitishwa huko Paris, Ufaransa mwaka jana na hivyo kuweka matumaini kuwa mkataba huo unaweza kuanza kutekelezwa mwaka huu.

Rais wa China Xi Jinping na Rais Barack Obama wa Marekani wamewasilisha nyaraka hizo kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon huko Hangzhou, China hii leo.

Ban amesema kwa China na Marekani kuchukua hatua hiyo aliyoiita ya kihistoria, ina maana kuwa sasa kuna nchi 26 ambazo zimeridhia zikiwa zinachangia asilimia 39 ya hewa  chafuzi hivyo…

(Sauti Ban)

“Sasa tunahitaji nchi zingine 29 zinazochangia asilimia 16 za uchafuzi wa hewa duniani ili mkataba wa Paris uanze kutekelezwa. Nina matumaini tunaweza kufikia lengo hilo kabla ya mwisho wa mwaka huu na kabla sijamaliza awamu yangu ya ukatibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.”

image
Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-moon (Kushoto) akiwa na Rais Xi Jinping wa China na Rais Barack Obama wa Marekani huko Hangzhou. (Picha:UN/Eskinder Debebe)
Kwa mantiki hiyo amewasihi viongozi hasa wa kundi la nchi 20, G20 waongeze mchakato wao wa kitaifa wa kuridhia ili matarajio ya Paris yageuzwe kivitendo kama vile ulimwengu unavyotaka.

Mkataba wa Paris utaanza kutekelezwa siku 30 baada ya angalau nchi 55 zinazochangia asilimia 55 ya hewa chafuzi duniani zitakuwa zimeridhia au kuwasilisha nyaraka zao za kukubali mkataba kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.