Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matokeo ya uchaguzi Gabon yaleta vurugu, Ban asikitishwa

Matokeo ya uchaguzi Gabon yaleta vurugu, Ban asikitishwa

Umoja wa Mataifa umetaka wanasiasa huko Gabon kuchukua hatua ili kurejesha utulivu baada ya ghasia zilizoibuka kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

Matokeo ya awali yametangazwa na wizara ya mambo ya ndani ya nchi ya Gabon, Ali Bongo, rais wa sasa akitangazwa kuwa ni mshindi, ambapo Katibu Mkuu  wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon amesema anafuatilia kwa makini matokeo hayo huku akieleza masikitiko yake kuhusu taarifa za uchomaji moto majengo na vurugu kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama kwenye mji mkuu Libreville.

Bwana Ban kupitia msemaji wake amewasihi viongozi  wote wa kisiasa na wafuasi wao kujizuia na vitendo vyoyote vinavyoweza kudidimiza amani na utulivu wa nchi.

Amevitaka vyombo vya usalama kuwa makini wakati wa kutuliza ghasia, pia waamdamaji  kutekeleza wajibu wao wa kuandamana bila kuhatarisha  amani.

Katibu Mkuu amemuomba  mwakilishi wake maalum kwa Afrika ya kati Abdoulaye Bathily kushirikiana na wadau wa kisiasa Gabon katika kutuliza hali ya sasa na kusaka suluhu ya masuala wanayozozana kwa njia ya amani.