Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asilimia 40 ya watoto katika nchi 10 watwama katika elimu

Asilimia 40 ya watoto katika nchi 10 watwama katika elimu

Watoto wakijiandaa kuanza mwaka mpya wa masomo, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema takriban watoto wawili kati ya watano kwenye nchi 10 zenye mizozo, hawaendi shuleni.Taarifa zaidi na Rosemary Musumba.

(Taarifa ya Rosemary)

UNICEF imesema hiyo ni sawa na watoto millioni 18 walio nje ya shule ambapo Liberia inaongoza  ikifuatiwa na Sudan Kusini ambapo karibu asilimia 59 ya watoto wanakosa haki yao ya elimu ya msingi kutokana na migogoro.

Katika taarifa yake, UNICEF imesema inahofia kuwa bila elimu, vizazi vijavyo vya watoto wanaoishi katika nchi zilizoathirika na vita, majanga ya asili na umaskini hawataweza kujimudu bila ujuzi na kuweza kuziendeleza nchi zao kiuchumi na hivyo basi kuzidi kuathirika.

Hata hivyo baadhi ya nchi zinazopokea wakimbizi kama Uganda, elimu imekuwa ikitolewa kwa watoto kama anavyoelezea Lisa Bender mtaalamu wa mipango ya elimu kwa nchi zenye majanga..

(Sauti ya Lisa)

“Ndio nimerudi hivi karibuni kutoka Uganda. Hii ni nchi ambayo imepokea wakimbizi wengi kutoka Sudan kusini na  hawa watoto wakimbizi wengi wanafurahia mno kuwa shuleni,  kukutana na marafiki wengine na kupata mafunzo.”

Nchi nyingine ambazo elimu kwa watoto ina mwamo ni Afghanistan,  Sudan,  Niger na Nigeria.