Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jeshi la Syria na ISIS walitumia silaha za kemikali- Ripoti

Jeshi la Syria na ISIS walitumia silaha za kemikali- Ripoti

Uchunguzi uliofanyika kwa ridhio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa umebaini kuwepo kwa matukio matatu ya matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria tangu mwezi Aprili mwaka 2014.

Uchunguzi huo huru na usiogemea upande wowote uliendeshwa na jopo la watu watatu kupitia mfumo wa uchunguzi wa pamoja, JIM ambapo waliangazia visa tisa vya matumizi ya silaha za kemikali na hivyo walipaswa kubainisha ni nani walitumia.

Virginia Gamba ni mkuu wa JIM na akihojiwa na Cristina Silveiro wa Radio ya Umoja wa Mataifa amesema..

(Sauti ya Virginia)

“Tulichofanya ni kubaini na kwa mantiki hiyo tumebaini wahusika: kimsingi ni wawili; jeshi la Syria hususan kikosi cha anga na mwingine ni ISIS hasa katika eneo la Marea ambako ni moja ya maeneo matatu ambayo yalibainika kuwa silaha za kemikali zilitumika. Taarifa hizi sasa ziko mbele ya Baraza la Usalama na ni juu yao kufuatilia mchakato wa uwajibikaji. Hatua ambazo zitafuata ni jambo ambalo wanapaswa kushughulikia.”

Bi. Gamba amesema kutokana na sababu za usalama na mashambulizi makubwa kwenye eneo la uchunguzi, si wao wala kundi la kusaka ukweli liliweza kuingia eneo husika.

 (Sauti ya Virginia)

“Lakini tuliweza kutuma makundi mengi, kutoka Damascus na nchi jirani na tulikuwa na ushahidi kupitia mahojiano ambayo tulifanya kutoka eneo husika na kwenye ukanda huo, halikadhalika kwa fomu tulizotuma kwa njia ya elektroniki.”

Hii ilikuwa ni ripoti ya tatu kuwasilishwa na jopo hilo mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.