Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko Myanmar kwa hatua za maridhiano- Ban

Heko Myanmar kwa hatua za maridhiano- Ban

Akiendelea na ziara yake huko barani Asia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekutana na kiongozi mshauri wa Myanmar Aung San Suu Kyi ambapo amesema wamejadili masuala kadhaa ikiwemo zahma inayokumba watu wa jamii ya Rohingya katika jimbo la Rakhine.

Katika mkutano na wanahabari uliofanyika mji mkuu Naypyidaw na kumjumuisha pia Bi. Aung, Ban amesema wamekubaliana kuwa wananchi wa Myanmar bila kujali kabila, dini au hali ya kiuchumi, wanahitaji fursa bora za kijamii na kiuchumi kwenye mazingira ambamo kwayo kila mmoja anakuwa huru, sawa na salama.

Hivyo amesema amemweleza hofu ya jamii ya kimataifa juu ya hali ya jamii hiyo ya Rohingya akisema kuwa ni changamoto ambayo hata Umoja wa Mataifa iko tayari kusaidiana na Myanmar kuitatua.

Amesema Umoja wa Mataifa unatiwa moyo na jitihada zilizochukuliwa na Myanmar ikiwemo kuanzisha tume inayoongozwa na katibu mkuu wa zamani Kofi Annan kuangalia suala la Rakhine.

Amepongeza serikali kwa hatua zilizochukuliwa ikiwemo uchaguzi wa kidemokrasia mwaka jana, lakini amesema hatua hizo zinahitaji kuimarishwa na hayo ndiyo matarajio ya jamii ya kimataifa.

Akiwa Myanmar, Ban atashiriki mkutano wa Panglong unaolenga kujadili mvutano wa kikabila uliokumba nchi  hiyo kwa miongo kadhaa sasa.