Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake na wasichana wenye ulemavu wanahitaji uwezeshaji, si huruma; CRPD

Wanawake na wasichana wenye ulemavu wanahitaji uwezeshaji, si huruma; CRPD

Wanawake na wasichana wenye ulemavu wanastahili kutambuliwa kama watu wengine na wawe na haki ya kujiamulia mambo kuhusu maisha yao .

Imesema kamati ya haki za watu wenye ulemavu , CRPD, ambayo leo imetoa mwongozo kwa mataifa 166 yaliyoridhia mkataba wa haki za watu wenye ulemavu ikisema wanachotakiwa kupatiwa ni haki na si huruma.

Mwongozo huo ambao lengo lake ni kusaidia kukuza uwezeshaji wa kundi hilo unatoa wito kwa nchi wanachama kubadili sera zinazowabagua.

Mathalani unamulika mambo matatu yanayotia wasiwasi kwa wanawake na wasichana wenye ulemavu, mosi ni ukatili wa kimwili, kingono , au kisaikolojia, pili haki za uzazi na kujamiiana , ikiwa ni pamoja na haki kubeba ujauzito, kuzaa na kulea mtoto; na tatu ni ubaguzi mbali mbali.

Kamati hiyo inasema ni matumaini yake kwamba nchi wanachama watatumia mapendekezo yaliyotajwa katika mwongozo huo katika kubadilisha sheria zao kuhusu haki za binadamu za wanawake na wasichana wenye ulemavu.