Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake na wasichana wapoteza muda mwingi kusaka maji- UNICEF

Wanawake na wasichana wapoteza muda mwingi kusaka maji- UNICEF

Wanawake na wasichana hupoteza jumla ya saa Milioni 200 kila siku wakisaka maji, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF katika taarifa yake ya kuanza kwa wiki ya maji inayoendelea hadi mwishoni mwa wiki.

Mkuu wa UNICEF anayehusika na kitengo cha maji, huduma za kujisafi na usafi Sanjay Wijesekera amesema saa hizo ni sawa na kusema tangu zama za mawe hadi sasa hakuna maendeleo kwenye sekta hiyo licha ya maendeleo makubwa ambayo ulimwengu unajivunia.

Kwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara wastani wa muda wa kusaka maji kijijinini dakika 33 ilhali mijini ni dakika 25, ingawa amesema kwa nchi kama Mauritania na Yemen muda ni mrefu zaidi.

Wijesekera amesema badala ya wanawake kutumia muda mwingi kuhudumia familia zao kwa masuala mengine muhimu, wanapoteza muda huo kusaka huduma hiyo ambayo ni haki yao ya msingi lakini bado imesalia ndoto kuipata.