Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Israel sitisha mipango ya ujenzi Yerusalem mashariki- Mladenov

Israel sitisha mipango ya ujenzi Yerusalem mashariki- Mladenov

Mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu mchakato wa amani mashariki ya kati, Nickolay Mladenov ameitaka Israel kuachana na mipango yake ya ujenzi wa makazi mapya kwenye eneo inalokalia la Palestina.

Amesema hayo wakati akiwasilisha ripoti yake kwa njia ya video kwa wajumbe wa Baraza la Usalama waliokutana leo kujadili hali ya mashariki ya kati hususan suala la Palestina.

Mladenov amesema tangu mwezi Julai Israeli imekuwa ikisongesha mipango ya kujenga nyumba 1,000 huko Yerusalem Mashariki na makazi mengine Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan.

(Sauti ya Mladenov)

“Hebu na nieleweke; hakuna sarakasi zozote za kisheria zinazoweza kubadili ukweli kwamba, iwe ni halali chini ya sheria za Israel, iwe kwenye eneo la nchi, ardhi isiyokaliwa au ardhi binafsi. Kama ilivyo kwenye maeneo ya walowezi ya eneo C au Yerusalem Mashariki, inasalia kuwa kinyume cha sheria chini ya sheria ya kimataifa. Ni vigumu kuelewa nia ya dhati ya vitendo hivi katika kuelekea suluhu ya mataifa mawili.”

Mratibu huyo amesema miaka 37 iliyopita Baraza la Usalama liliazimia kuwa makazi ya Israeli kwenye eneo inalokalia la Palestina hayana uhalali wote na ni kikwazo kwa amani ya kudumu Mashariki ya Kati, na kwamba uamuzi huo unasalia na ukweli hata hii leo.