Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ofisi ya haki za binadamu yalaani kunyongwa kwa watu 12 Iran

Ofisi ya haki za binadamu yalaani kunyongwa kwa watu 12 Iran

Vita dhidi ya madawa ya kulevya, haihalalishi matumizi ya hukumu ya kifo kinyume cha sheria, amesema mtaalamu maalum wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Iran, Ahmed Shaheed.

Ametoa kauli hiyo baada ya kukasirishwa na kitendo cha kunyongwa kwa watu 12 mmoja wao akiwa ni Alireza Madadpour mnamo Agosti 27 nchini Iran.

Amesema kunyongwa kwa watu hao kulifanyika licha ya kukata rufaa kwa mamlaka za Iran akitaka kutoendelea kwa mpango huo wa mauaji katika gereza kuu la Karaj.

Bwana Shaheed amesema kitendo hicho ni kinyume cha sheria na kwamba sheria ya kimataifa inasema hukumu ya kifo itolewe katika  kesi zenye uhalifu wa hali ya juu mfano mauaji ya kukusudia, na pale ambapo mkono wa sheria umeamua kwa haki, fursa ambayo amesema Alireza Madadpour hakupatiwa.

Mtaalamu huyo amesema mauaji hayo yanaonyesha dharau ya mamlaka ya Iran katika wajibu wake chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu.