Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki za wafanyakazi wahamiaji zilindwe bila kujali hadhi zao- Kamati

Haki za wafanyakazi wahamiaji zilindwe bila kujali hadhi zao- Kamati

Kamati ya ulinzi wa haki za wafanyakazi wahamiaji imeanza kikao chake cha 25 hii leo huko Geneva, Uswisi ambapo imeelezwa kuwa mfumo mpya unahitajika duniani katika  kushughulikia wimbi kubwa la mienendo ya wakimbizi na wahamiaji.

Akisoma taarifa yake wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Ibrahim Salama mkuu wa mikataba ya haki kutoka ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa amesema mfumo huo mpya unapaswa kutetea haki za makundi hayo bila kujali hadhi zao.

Kwa mantiki hiyo amesema ofisi ya haki za binadamu inapendekeza mambo matatu ambayo yanapaswa kupatiwa kipaumbele wakati wa mkutano wa ngazi ya juu kuhusu wakimbizi na wahamiaji utakaofanyika New York, Marekani mwezi  ujao..

(Sauti ya Ibrahim)

“Mosi kipaumbele cha haki za binadamu, pili kwa sababu ya mazingira ya wimbi hili la mwenendo wa watu, ni lazima suala hili litekelezwe kwa mtazamo wa haki za binadamu, na tatu kuna uharaka wa kuwepo kwa mfumo wa kina wa masuala ya uhamiaji na usakaji uhifadhi unaozingatia haki za binadamu.”

Bwana Salama amesema kutokana na ukosefu wa uelewa kuhusu viwango vya kulinda haki za wahamiaji wanapokuwa kwenye wimbi hilo la kuhama, ofisi ya haki za binadamu inaanda muongozo ambao utalinda haki zao kwenye mazingira ambamo kwayo wanaenguliwa na kukosa haki kama wapatazo wakimbizi.