Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tushikamane tutekeleze mkataba dhidi ya nyuklia- Ban

Tushikamane tutekeleze mkataba dhidi ya nyuklia- Ban

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kupinga majaribio ya silaha za nyuklia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametaka kuwepo kwa mshikamano ulimwenguni ili kutokomeza mkwamo katika kufikia azma ya dunia isiyokuwa na silaha za nyuklia.  Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

Katika ujumbe wake Ban amesema mshikamano na utashi wa kisiasa vimejidhihirisha kuwezekana katika masuala magumu ikiwemo kupitisha ajenda ya maendeleo endelevu, hivyo ametaka mshikamano huo utumike kukamilisha uridhiaji wa mkataba dhidi ya majaribio ya silaha hizo uliopitishwa na Umoja wa Mataifa miaka 20 iliyopita, ili hatimaye uanze kutumika.

Lassina Zerbo, ni katibu mtendaji wa tume ya maandalizi ya mkataba huo.

(Sauti ya Lassina)

“Hivi nchi nane ziendelee kuzuia dunia nzima kwa muda wote huu? Kuna jambo linapasaw kufanyika.”

Karipbek Kuyukov ni mhanga wa majaribio ya nyuklia huko Kazakhstan na alizaliwa bila mikono lakini sasa anatumia kipaji chake cha kuchora kueneza ujumbe wa madhara ya silaha hizo.

(sauti Kuyukov)

“Nilizaliwa bila mikono, lakini nadhani kila mtu anakabili maisha kadri azaliwavyo. Nilifanya kila kitu kwa kutumia miguu yangu. Nilipokuwa mtoto nilichora kwa kutumia vidole vya mguu na nikaanza kuchora vitu rahisi, picha, na kadri nilivyokua, niliendelea kupenda. Ninachora ili watu waweze kutazama na wafikirie kwa nini watu wanapaswa kutaabika na janga hili?”