Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunasubiri uamuzi, tuko tayari kupeleka msaada Aleppo-De Mistura

Tunasubiri uamuzi, tuko tayari kupeleka msaada Aleppo-De Mistura

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Steffan de Mistura ametoa wito leo kwa wahusika wote katika mzozo wa Syria kutumia nguvu na ushawishi kuhakikisha msaada wa kibinadamu ulio tayari unawafikia watu Aleppo walio katika hatari kubwa.

Wito huu unafuatia ombi la wiki iliyopita la kusitisha mapigano kwa saa 48 kila juma ambalo pia ulikaribishwa na kuungwa mkono na Urusi na amesema Umoja wa Mataifa umeweka tayari mpango wa dharura ambao utasaidia watu 80,000 wa Aleppo na uko tayari kukarabati mfumo wa umeme utakaosaidia watu milioni 1.8.

Amesema anafahamu wasiwasi wa pande kinzani kuhusu matumizi ya barabara ya Castello kusafirisha msaada Aleppo, lakini ana matumaini kuwa mazungumzo yanayoendelea yatazaa matunda mazuri, kwani hii ndio njia chanya pekee iliyobainiwa na Umoja wa Mataifa kuendesha operesheni hii kwa mara ya kwanza.

Bwana de Mistura amesema juhudi bado zinaendelea baina ya Marekani na wadau wote wa masuala ya kibinadamu kuhakikisha kuna muafaka wa kuanzisha operesheni hii na anatumai ifikapo Jumapili ya Agosti 28 atajua kuna msimamo upi, na anasisitiza kutokuwepo kwa mapigano ndani na karibu na eneo la sitisho.

Amekumbusha pande husika kwamba Umoja wa Mataifa uko tayari na kwamba hakuna tena muda wa kusubiri kwa kuwa watu  wa Aleppo wanateseka.