Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufyatuaji kombora wa DPRK unadumaza hali ya wananchi- UM

Ufyatuaji kombora wa DPRK unadumaza hali ya wananchi- UM

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani vikali ufyatuaji kombora kutoka kwenye nyambizi kulikofanywa na Jamhuri ya watu wa Korea DPRK tarehe 23 mwezi huu.

Katika taarifa yake, baraza hilo limesema kitendo hicho ni miongoni mwa matukio ya urushaji wa makombora na majaribio ya silaha za nyuklia, ambayo ni  kinyume na sheria za kimataifa na wito wa mara mwa mara wa jumuiya ya kimataifa wa kupinga tabia hizo.

Halikadhalika Baraza la Usalama limesema msururu huu wa matumizi ya silaha unaofanywa na DPRK ni kinyume na maazimio kadhaa ya baraza hilo.

Baraza hilo limesema pamoja na kukiuka sheria na maazimio, vitendo hivyo vinaleta mvutano na wasiwasi mkubwa katika rasi ya  Korea, kanda, na dunia nzima, na vitendo hivyo pia ni matumizi yasiyo sahihi ya rasilimali kwa watu  wa DPRK ambao wanaishi katika hali duni.

Kwa mantiki hiyo wanachama wa baraza wamesisitiza umuhimu wa kushirikiana katika kupunguza mvutano katika rasi ya Korea na kwingineko na utayari wao wa kufuatilia hali hii kwa ukaribu zaidi na kuchukua hatua madhubuti zaidi sambamba na dhamira za hapo awali.