Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kauli ya UNICEF baada ya sitisho la mapigano Aleppo

Kauli ya UNICEF baada ya sitisho la mapigano Aleppo

Leo ni siku nyingine ya majonzi na hatari kwa watoto huko nchini Syria hasa wale wanaoishi mji wa Aleppo.

Hiyo ni kauli ya Antony Lake Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF aliyotoa hii leo baada ya tangazo la sitisho la mapigano kwa ajili ya kufikisha misaada ya kibinadamu mjini humo.

Katika taarifa yake Bwana Lake amesema hivi sasa watoto takriban 100,000 wamezuiliwa mashariki mwa mji huo tangu mwezi Julai mwaka huu huku watu zaidi ya 35,000 wakiwa wamekimbia makazi yao katika sehemu ya magharibi.

Amesema UNICEF iko tayari kutoa misaada kwa haraka, ikiwemo dawa, chanjo na chakula cha kuongezea watoto nguvu, halikadhalika kufanya tathmini na ukarabati wa vifaa muhimu vya umeme na kutoa maji safi na salama ya kunywa

Akiongezea, mkurugenzi huo amesema, watoto wa Aleppo hawapaswi kuendelea kuishi kwa hofu mashambulizi, akiutaja Aleppo kuwa mji wenye hatari zaidi duniani.

Bwana Lake amesema kuna umuhimu wa kusitisha mapigano hadi pale amani inapatikana na ili kuwezesha misaada kupenya na hivyo kuokoa maisha ya walioathirika.