Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP na operesheni ya dharura Uganda kukwamua wakimbizi

WFP na operesheni ya dharura Uganda kukwamua wakimbizi

Shirika la mpango wa chaukula duniani, WFP, limeanzisha operesheni ya dharura nchini Uganda kusaidia maelfu ya wakimbizi waliokimbia mapigano mapya Sudan Kusini.

WFP imesema ongezeko kubwa la wakimbizi nchini Uganda limetokana na mapigano ya mwaka 2013 Sudan Kusini, pamoja na mgogoro wa hivi karibuni nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mike Sackett, ni Mkurugenzi wa WFP nchini Uganda

(Sauti ya Mike)

"Uganda imekaribisha idadi kubwa ya wakimbizi , karibu nusu milioni , kutoka Burundi, DRC lakini hasa kutoka Sudan Kusini ambayo imeathirika zaidi na mapigano makubwa sana kuanzia mwishoni mwa mwaka 2013 , lakini pia mwezi uliopita. "

Kutokana na upungufu wa fedha, WFP imelazimika kukata mgao wake kwa wakimbizi waliowasili nchini Uganda kabla ya Julai, 2015, hatua ambayo itaathiri nusu ya idadi nzima ya wakimbizi nchini humo.

Wakimbizi wanaowasili baada ya hapo hasa wazee, yatima na waliokumbwa na utapiamlo watapata mgao kamili.